full screen background image
Safari Trippers at their best

IMETIMIA MIAKA 22 TOKA KIFO CHA NGULI MARIJANI RAJABU

 

ALHAMISI, Machi 23 mwaka 1995 ni siku isiyosahaulika kwa wapenzi wa muziki wa zamani
nchini. Siku hiyo ndipo tulipompoteza mwanamuziki kipenzi chetu, Marijani
Rajabu. Alizikwa kesho yake Ijumaa Machi 24 kwenye makaburi ya Kisutu.

 

Historia ya gwiji huyu inaanzia siku alipozaliwa tarehe 3 Machi mwaka 1955, katika eneo
la kariakoo.  
Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa
Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia.
 Alisoma shule ya Msingi ikiambatana na
elimu ya Madrasa.  
 Mwaka 1970 Akiwa bado shuleni, utaona umri wake ulikuwa miaka 15 tu,  alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips., hili jambo la mwanafunzi kusafiri na bendi likaleta shida na kwa
vile STC ilikuwa mali ya umma akaachishwa kazi na
mwaka1972 alijiunga na The Trippers ya David Mussa ambayo kwa wakati huo ilikuwa inapiga zaidi nyimbo za hoteli na za kukopi na muimbaji wao kiongozi wakati huo alikuwa Ali Rajabu. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Trippers, ambayo sasa ilibadili jina na kuwa Safari trippers kutokana na msimamo wa serikali wakati huo wa kutaka majina ya nyumbani yatumike bala ya yale ya kigeni na  kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchI nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake
vizuri.

Safari Trippers at their best

Safari Trippers at their best

Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati
bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo
. Marijani
alishiriki kutunga, kuimba nyimbo karibu zote za Trippers sanjari na kupiga
gitaa kwa baadhi ya nyimbo. Mfano wimbo Olila ambao alipiga rhythm na kuimba.

Mwaka 1976, Marijani na baadhi ya wanamuziki wa Trippers waliamua kuihama bendi na
kwenda baadaye kuasisi Dar es salaam International chini ya umiliki wa Mzee
Zakaria Ndabemeye ambaye bado yu hai hadi sasa. Baadhi ya wanamuziki hao ni
pamoja na Abel Baltazar kutoka Msondo, Kassimu Mponda kutoka Trippers, Abdallah
Gama, Joseph Mulenga, Haruna Lwali na George Kessy Omojo waliokuwa wanapiga
muziki Magot pale, Said Mohamed kutoka Polisi Jazz, Cosmas Chidumule kutoka Urafiki,
Belesa Kakere kutoka Biashara Jazz, Joseph Bernard kutoka Trippers, Ali Rajabu
kutoka Trippers, na King Michael Enock kutoka Dar es salaam Jazz. Akiwa Dar
Inter alishiriki kutunga nyimbo mbili, Betty na Sikitiko. Hata hivyo kama
waswahili wanavyosema mafahari wawili hawakai zizi moja ndivyo ilivyotokea kati
yake na Abel Balthazal kiasi cha hatimaye Marijani kufukuzwa ndani ya bendi
kutokana na ubishi kuhusu wimbo aliotunga Marijani, kuna maelezo kuwa wimbo
ulionekana unafanana na wimbo fulani toka Kongo na hivyo Marijani akatakiwa
aubadilishe na ndipo ugomvi ukaanza. Hata hivyo mwishoni mwa mwaka 1978,
Marijani alirejeshwa tena kundini kutokana na rundo la wanamuziki wa Dar Inter
kuihama bendi kwa kishindo kikubwa na kwenda kuifungua bendi mpya kabisa ya
Orchestra Mlimani Park. Aliporejeshwa Marijani alikuja na wanamuziki wengi
wapya wakati huo kama akina Christopher Kasongo, Mohamed Tungwa, Mafumu Bilal,
Hamis Milambo, Athuman Momba, Mzee Alex Kanyimbo na wengine na kuja na mtindo
wa Super Bomboka. Katika kudhihirisha hasira zake kwa Abel, Marijani alimtungia
Abel wimbo wa kumnanga ukiitwa Kidudu mtu ambao hata hivyo RTD waliukataa
kuurekodi, jambo lililokuwa kawaida enzi hizo kwa redio kukataa wimbo. Sifa
nyingine ambayo Marijani alikuwa nayo ni kuibua wanamuziki chipukizi kama
alivyofanya mwaka 1983 alipomuibua kutoka Tanga kijana Mkuu Waziri Kungugu
Kitanda Milima almaaruf Fresh Jumbe ambaye kwa hakika kabisa Marijani hakujutia
kumchukua kijana huyo. Alimuamini kupita maelezo kiasi kwamba wakati mwingine
alikuwa akimuachia bendi aongoze na yeye anapumzika nyumbani. Mbali na Fresh,
wanamuziki wengine ni kama vile Tino Masinge, Mohamed Mwinyikondo, Juma Choka
na wengine kibao. Ni vizuri kuelezea hapa kuwa kadri ya maelezo yake mwenyewe
marehemu  baada ya kurekodi
Zuena na Mwanameka na nyimbo nyingine katika album hiyo alichoambulia ni malipo ya nauli toka RTD ya sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao.
Hata hivyo safari ya Dar International ilikoma mwaka 1987 kutokana na sababu za
kawaida za kufa kwa bendi lakini kubwa ni uchakavu wa vyombo. Hata hivyo
Marijani aliendelea kufanya muziki na kwa kipindi kifupi amewahi kucheza na
Kurugenzi ya Arusha na Mwenge Jazz ambayo alirekodi nayo wimbo mmoja wa Ukimwi
na hata kupitia bendi ya Watafiti ambayo hatimae ilikuja kuwa 38.. Mwaka huohuo
wa 1987 Marijani na Muhidin Maalim Gurumo waliliongoza kundi la wanamuziki
zaidi ya 50 kutunga nyimbo maalum hasa kwa maadhimisho ya miaka 10 ya CCM na 20
ya Azimio la Arusha. Naizungumzia Tanzania All Stars. Aidha mwaka 1994 aliwahi kurekodi
zong zing na marehemu Eddy Sheggy. Bendi yake ya mwisho ilikuwa ni Africulture
ama Mahepe Ngoma ya Wajanja, iliyokuwa mali ya Rogers Malila, alikokuwa na
wanamuziki kadhaa kama akina  Hassan Kunyata, Mgosi na wengine. Bado
Marijani ataendelea kukumbukwa na wapenda muziki kote nchini na hata Afrika kwa
ujumla kwa nyimbo zake zenye mafundisho na tamu huku akienzi utamaduni na ngoma
za kwao Kigoma.
ANGALIA VIDEO MARIJANI LIVE
3 thoughts on “IMETIMIA MIAKA 22 TOKA KIFO CHA NGULI MARIJANI RAJABU

 1. Ali Said

  Dear Mzee Kitime,
  Shukran kwa makala hii muhimu kuhusu mmoja wa magwiji wa muziki wa Africa.
  Hapo Tz,Marijani ndie aliyerithi ustadi kutoka kwa Mbaraka Mwinshehe Mwaruka kama vile Mbaraka nae alivyorithi toka kwa Salum Abdallah,na Mwenyezi mungu awarehemu wote watatu.
  Kwa lugha ya hapa ninapoishi Englang,hawa hote walikuwa ma Genius katika fani yao.
  Kitu cha kusikitisha ni kuwa hawa wote walikufa masikini,can you really believe it?
  Mbaraka Soloist Nation,Marijani Jabali la muziki..inatia uchungu mkubwa sana,sana.
  Huku Europe ninapoishi,wanathimini magwiji wao wote waliopita miaka mamia kadhaa iliyopita kama Mozart,Bach,Beethoven etc.
  Hapa England,uko uwanja mkubwa wa ndege unaitwa John Lenon,aliyekuwa wa the Beatles.
  Kufa maskini na kudharauliwa na kutojaliwa kwa hawa ma Genius ni hukumu ya wazi ya jinsi gani watu wa kwetu walivyo nyuma kifikra na katika ustaarabu,kwani asiyethamini mila na utamaduni wake ni mtumwa tu..
  Nina uhakika hakuna Gazeti lolote au TV Station yoyote huko Tz ililioadhimasha hii miaka 22 toka Marijani atutoke kama ulivyofanya wewe hapa,shukran nyingi za dhati kutoka kwangu hapa London,England.
  Angalia,hakuna hata mtu mmoja aliyeacha comment hapa juu ya makala yako muhimu..
  Wewe ndie peke yako uliyoweka Live recording ya Marijani kwenye You Tube miaka michache iliyopita,hivi ni kweli hakuna mwingine mwenye video za Jabali Marijani,lakini hawajali au kwa lugha ya hapa ni kuwa they dont give a damn!!
  Heshima yangu juu yako,iko juu sana,na mwenyezi mungu akujalie afya njema ili uzidi kuwatendea haki hawa ma Genius ambao lazima vizazi vijavyo vije viwajue otherwise,as I said earlier,a person without culture/history is a slave…
  Thank you so much.
  Pleasae,tafuta video nyingine za Marijani na utuwekee..just imagine watching Jabali akiimba Siwema…

  Warm Regards

  A Said

  Reply
 2. Original Trippers Fan

  Rest in peace dear DAVID GORDON… and other Safari Trippers band members who passed away over the years.

  Reply

Leave a Reply

Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com
%d bloggers like this: