full screen background image
chuck-berry-new-album-news-2a7vc3dn

MAGWIJI HAWA WAMETUTOKA LAKINI KAZI ZAO ZINAISHI

KILA JUMAMOSI MAKALA KAMA HII HUTOKA KATIKA GAZETI LA MWANANCH… USIKOSE

Mwaka 2017 umeanza kwa matukio ya huzuni katika tasnia ya muziki wa dansi. Wanamuziki kadhaa wakongwe wamefariki akiwemo mwanamuziki wa Afrika ya Kusini Joe Sdumo Mafela aliyeimba wimbo wa Shebeleza, ambaye amefariki siku chache zilizopita tarehe 18 March, kutokana na ajali ya gari. Joe alizaliwa 1942. Lakini leo ntaongelea wanamuziki wawili ambao kwa umahiri wao waliweza kubadilisha muziki katika kila kona ya dunia. Wanamuziki hao ni mpiga drums Clyde Stubblefield na mpiga gitaa Chuck Berry. Si majina ambayo ni maarufu hapa, lakini kuna mambo wanamuziki wetu wanayafanya ambayo chanzo chake ni wanamuziki hawa wawili. Wanamuziki wote niliowataja hapo juu ni Wamarikani weusi.

Picks-Clyde-Stubblefield-11192015

CLYDE STUBBLEFIELD

Clyde Stubblefield alikuwa mmoja ya wapiga drum wawili wa kundi la Famous Flames lililokuwa likiongozwa na mwanamuziki maarufu, marehemu James Brown, aliyefariki siku ya Krismas mwaka 2006, ambae nae kazi zake zinaendelea kuigwa mpaka leo na wanamuziki wa sasa. Clyde aliyefariki Februari 18 mwaka huu kutokana na matatizo ya figo, alizaliwa tarehe 14 April, 1943. Alijifunza mwenyewe kupiga drums, aliwahi kusema alikuwa akisikiliza sauti mbalimbali zilizokuwa zikimzunguka na hivyo kutunga mapigo mbalimbali. Awali alikuwa mpiga drum katika band ya muimbaji mwingine maarufu marehemu Otis Redding na hatimae mwaka 1965 akajiunga na kundi la James Brown. Alidumu katika kundi hili mpaka mwaka 1971, kati ya kazi alizozifanya katika kipindi hiki zinasikika katika nyimbo maarufu za bendi hiyo kama Cold sweat, Say it Loud I’m Black and Proud, na I got a feeling.

Lakini kwa kazi hizi aliweza kubadili muziki wa bendi nyingi duniani ikiwemo za Tanzania. Bendi nyingi za rumba kabla ya mwaka wa 70 zilikuwa hazitumii drums, katika tungo zao, bendi zilikuwa na chombo hicho lakini mara nyingi kilitumika kwa nyimbo ambazo si tungo za bendi. Katika miaka hiyo bendi kubwa za Kongo zilianza kutumia chombo hicho kwenye tungo zao. Tabu Ley na kundi lake la Orchestre Afrisa International akaja na mtindo wake wa Soum Djoum ambao mipigo ya drums ilikuwa ikifuata mipigo ya drums alizotunga Clyde na hapo likafunguka pazia la bendi kila kona ya Afrika kupiga muziki na kuingiza vipande vya mipigo ya Clyde. Wimbi hilo pia liliwakumba wanamuziki wa hapa kwetu. Kati ya nyimbo ambazo ziliiga moja kwa moja mapigo hayo ni Morogoro Jazz Band. Ukisikiliza wimbo wake, Enyi vijana sikilizeni, uliokuwa ukiwaasa wanafunzi wazingatie masomo na kutojihusisha na mapenzi, katikati ya wimbo huu waliingiza kipande ambacho Clyde alikipiga katika wimbo Make it Funky wa Famous Flames. Bendi nyingi sana zilijikuta zikitumia

mapigo yale. Ubunifu wa Clyde haukuishia kuathiri bendi za rumba tu, kwani hata zama hizi, hapa kwetu na duniani kote wasanii wa Hip hop wamekuwa wakitengeneza ‘beat’ kutumia kazi ya Clyde. Kazi za mpiga drum huyu imetumika kama beat kwenye za hiphop za kundi la Public Enemy, NWA na hata kazi za Dr Dre, hawa ni wasanii wa Hiphop wenye umaarufu dunia nzima. Kwa takwimu rasmi, drum aliyopiga Clyde katika wimbo Make it Funky, imeshatumika katika zaidi ya nyimbo 1000 na wasanii mbalimbali wa Kimataifa, hakika hesabu hii hazijajumlisha matumizi katika kazi za nchi zinazoendelea ambako beat hiyo bado inaendelea kutumika.

chuck-berry-new-album-news-2a7vc3dn

Mwanamuziki mwingine ni Chuck Berry. Chuck aliyekuwa mpiga gitaa ambaye hupewa sifa ya kuwa muasisi wa mtindo wa Rock’n’ Roll, amefariki tarehe March 18, 2017. Chuck alirekodi nyimbo yake ya kwanza Maybellene mwaka 1955, akafuatia na Roll over Beethoven mwaka 1956, Johnny Be Goode mwaka 1958. Kujua kupiga nyimbo hizo ilikuwa kama ndio kipimo cha kwanza cha kujua kupiga muziki wa Rock n Roll. Makundi maarufu ya muziki huo kama vile Beatles na Rolling Stones yote yalirekodi upya nyimbo za Chuck miaka mingi baada ya kurekodiwa nyimbo ya awali, na hata leo nyimbo hizo zinaendelea kupigwa majukwaani. Wapiga magitaa wa muziki wa rock wote husema walianza kwanza kwa kujifunza kupiga nyimbo za mkongwe huyu ambaye hakika katika ujana wake alikuwa na vituko vingi kiasi cha kujikuta gerezani zaidi ya mara mbili, mara ya kwanza kwa kosa la kufanya mapenzi na binti wa miaka 14, na mara nyingine kwa kukwepa kodi. Upigaji gitaa wa mwanamuziki huyu uliigwa pia na bendi zetu ambazo zilikuwa zikipiga muziki wa rock, lakini hata wapigaji ambao hawakupiga muziki huo walichukua staili yake na kuingiza katika muziki wao. Wakati wa umaarufu wa muziki wa twist, staili ya upigaji wake ilitumika sana. Jambo jingine kubwa ambalo baadhi ya wapiga magitaa wa rumba waliliiiga kutoka kwa mwanamuziki huyu ni kucheza wakati wa kupiga gitaa. Alikuwa na kila aina ya vituko awapo jukwaani na kuweza kucheza sana huku akifuata mapigo ya gitaa lake. Ni nadra sana kukuta wapiga magitaa wakitawala jukwaa siku hizi. Mungu awalaze pema wakongwe hawa. MUZIKI WAO UNAENDELEA KUISHI
Leave a Reply

Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com
%d bloggers like this: