full screen background image
MAROMBOSO MSHEDEDE2

MAROMBOSO MSHEDEDE,MUIMBAJI WA YAMOTO BAND

Maromboso Mshedede JINA lake kamili ni Mbwana Yussuph Kilungi lakini ukimtafuta kwa jina hilo unaweza usimpate kutokana na watu wengi hivi sasa, hususan mashabiki wa muziki, kumzoea kwa jina la ‘Maromboso Mshedede’.
Chanzo cha jina ‘Maromboso’, kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe, aliwahi kutengeneza wimbo alioupa jina hilo ili kuwa tofauti na wasanii wengine, lakini badala yake watu walipousikia wakawa yeye ndio wanamwita hivyo.
Awapo jukwaani, Maromboso ambaye ni kati ya waimbaji wanne wa Yamoto Band, huonekana kuwa ni kijana machachari na mcheshi kwa mashabiki, ambapo muda wote hujaa maneno ya kuchekesha yanayomfanya asichokwe anapozungumza.
Mbali ya hilo, Maromboso pia amejaaliwa vipaji vya unenguaji na uimbaji ambavyo kadhalika, navyo humfanya azidi kuonekana ‘asali’ kwa mashabiki na wapenzi anapopanda jukwaani.
Katika vibao vyote vya Yamoto Band, sauti ya Maromboso huonekana kama chumvi inayoongeza utamu na kutia hamu kwa mtu anayesikiliza ama kumtazama laivu jukwaani.
“Nilianza kujiingiza kwenye muziki tangu nikiwa shule ya msingi, kwa kujihusisha na fani za Ngonjera, Jiving, Kwaya pamoja na sanaa nyingine mbalimbali za kishule,” anasema Maromboso.
Maromboso anasema kuwa, alipoingia sekondari akazidisha umakini kwenye sanaa, ambapo licha ya kuwachahafya wanafunzi aliokuwa akisoma nao, alikuwa pia anaiwakilisha shule yake katika mashindano malimbali ya nje, yakiwamo UMISSETA.
MAROMBOSO MSHEDEDE2

Wakati akiwa kidato cha pili, ndipo alipokwenda kwenye kituo cha Mkubwa na Wanawe kufanya usaili na kubahatika kuwa mmoja wa vijana wawili waliopita kwa kishindo kati ya wasanii 25.
Anamtaja msanii mwingine waliyepita nae pamoja kwenye usaili huo uliofanyika katika tarehe ambayo ni siku yake ya kuzaliwa, yaani Oktoba 3, ni ‘Dick’ ambaye hayuko katika taasisi ya Mkubwa na Wanawe.
“Hadi kufikia sasa, kiukweli kabisa tayari Mkubwa na Wanawe imeshanifanyia mengi kimaisha, ikiwa ni pamoja na kuniweka kwenye ramani ya wasanii wenye majina hapa nchini,” anasema Maromboso.
Maromboso anasema kuwa, ingawaje kila jambo linapangwa na Mungu, lakini ana hakika kabisa kuwa, kama isingetokea kuchukuliwa na Mkubwa na Wanawe, hivi sasa asingekuwa na mafanikio aliyonayo.
Anasema, hadi kufikia hapo alipo anawashukuru Said Fella ‘Mkubwa’ pamoja na Yussuf Chambuso kwa kuhakikisha wanafanya jitihada za makusudi katika kumuinua kiuimbaji.
Anasema kuwa, maombi na ushirikiano wa dhati baina yao wasanii wa Yamoto, ndio siri pekee ya mafanikio ya bendi hiyo ambayo waimbaji wake wengine ni Beka Flavor, Dogo Aslay na Enock Bella.
“Kikubwa zaidi ninachoshukuru ni namna sisi wasanii wa Yamoto Band tunavyopendana na kila mmoja kumuona mwenzie kuwa ni msaada mkubwa kwake,” anasema Maromboso.
Akielezea namna anavyokitunza kipaji chake cha uimbaji, Maromboso anasema kuwa, pamoja na mambo mengine, huchukua muda mrefu katika kulala na kufanya mazoezi ya sauti.
Kusikiliza nyimbo za wasanii wakubwa na wenye majina, hususan kutoka Marekani, Kongo (DRC) na Nigeria, ni kati ya mambo anayopendelea msanii huyo, ili kukuza upeo wake kimuziki.


TAG


2 thoughts on “MAROMBOSO MSHEDEDE,MUIMBAJI WA YAMOTO BAND

Leave a Reply

Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com
%d bloggers like this: