full screen background image
17

MCHANGO WA SERIKALI UWAPI KATIKA KUKUZA NA KUENDELEZA SANAA?

Nilikuwa naangalia filamu moja ya vichekesho ya Kinaijeria, katika filamu hii kulikuwa na familia yenye watoto wawili watukutu sana. Ikafikia baba kuanza kudai kuwa watoto wale si wake, na akawa akimlazimisha mkewe amtafute baba halisi wa watoto wale. Siku moja wakiwa katika ubishi huo, afisa kutoka kampuni ya bahati nasibu aliingia na kuwataarifu wazazi kuwa mmoja ya watoto wale alicheza bahati nasibu na alishinda mamilioni ya shilingi. Hapo hapo hali ikabadilika, yule baba akaanza kusifu akili za wanawe na kudai kuwa wamerithi akili toka kwake, na kwa kweli baada ya hapo baba yule alikuwa akipita mitaani kusifia jinsi malezi yake yalivyofanikisha watoto wake kuleta utajiri. Muvi ile imenikumbusha sana uhusiano kati ya serikali ya Tanzania na wasanii wa Tanzania. Sio siri kuwa kwa sasa serikali ina mchango mdogo sana katika kuhifadhi na kukuza sanaa nchini, lakini kuna historia iliyofikisha hali hii. Mwaka 1995, mara baada ya kuingia awamu mpya ya serikali, lilitangazwa baraza la Mawaziri, katika matangazo yale neno Utamaduni au Sanaa halikusika. Wasanii tulianza kujiuliza Je, tuko wapi? Hata maofisa wa utamaduni waliokuwa na nyadhifa kubwa serikalini hawakuwa na majibu. Kwa vile kabla ya awamu hiyo kulikuwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni basi ikategemewa kwa mazoea hali itaendelea vilevile. Baada ya muda mfupi ikawa wazi kuwa mambo yamebadilika, Maafisa Utamaduni wa Mkoa na hata Wilaya wakaondolewa kwenye ramani. Baada ya kipindi cha sintofahamu, Maafisa Utamaduni Wilaya wakaanza kurudi taratibu lakini, Maafisa Utamaduni wa awamu hii walikuwa wakiteuliwa na Afisa Elimu, na hivyo kuwa chini ya Idara ya Elimu katika maeneo yao. Wengi walikuwa waalimu, ajira yao ilikuwa ualimu japo cheo chao kilikuwa Afisa Utamaduni. Kwa mfumo huo kila Wilaya ikawa na taratibu zake kwani Maafisa hawa hawakuwa chini ya Wizara ya Utamaduni. Na ndio hali ilivyo hadi leo, Maafisa Utamaduni hawako wizara ya utamaduni bali wako TAMISEMI. Kutokana na Maafisa Utamaduni kuweko chini ya Idara ya Elimu, Utamaduni hauna nafasi yoyote ya maana, hauna fungu la matumizi, asilimia kubwa ya Maafisa hawa hawashiriki katika vikao vyovyote vya Halmashauri, hivyo halamashauri hazina mipango yoyote kuhusu Utamaduni na sanaa katika maeneo yao. Kulikuwepo hata fununu ya mpango wa kufuta kabisa Maafisa Utamaduni. Kwa mfumo huu ambapo Wizara ya Utamaduni inategemea Maafisa Utamaduni wasiothaminika walioko TAMISEMI, ni wazi kuwa sera za Wizara ya Utamaduni hazitatekelezwa, mipango ya Wizara hiyo haitatekelezeka, na hapo ndipo narudia kusema serikali ina mchango mdogo sana katika kuendeleza sanaa nchini. Lakini kama ilivyokuwa kwa wale wazazi wa ile muvi ya Kinaijeria, serikali huwa ya kwanza kujipongeza kwa msanii aliyeweza kujitokeza na kufanya jambo ambalo ni zuri. Katika mazingira ya serikali kutokuweko katika nafasi yake, maendeleo ya sanaa yamebebwa na wafanya biashara. Biashara nia yake kubwa huwa kupata faida, si kulinda kuhifadhi na kuendeleza sanaa, biashara pia haijibani kwa kuangalia maadili ya Taifa. Matokeo ya hali hii iko wazi kwa kila mtu. Lakini matokeo ya kazi ya wafanyabiashara ya sanaa yameanza kukumbatiwa na serikali kuwa ni maaendeleo ya sanaa!!!

Pamoja na maelezo yote ambayo hutolewa kuwa wakoloni walikuwa na nia ya kuuwa utamaduni wetu, hakika enzi za Ukoloni kulikuwa na jitihada zaidi za kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wetu kuliko hali ilivyo sasa. Yako wapi majengo ambayo yalijengwa na WAKOLONI (community centers), sehemu ambazo zilikuwa ni za kufanyia shughuli za Utamaduni? Katika Jiji la Dar, yamebadilishwa na kuwa kumbi za mikutano za viongozi wa Serikali za Mitaa, katika miji mingine majengo haya yamegeuzwa ofisi au kukodishwa kwa wafanya biashara. Hakujajengwa kitu chochote mbadala, japo ni katika vikao vinavyofanyika katika majengo hayo ndipo wasanii huambiwa atafute sehemu za kufanyia kazi zao. Ni jambo la kawaida sana viongozi kuhamasisha kujengwa viwanja vya michezo, husikii sauti za kuhamasisha kutengeneza maeneo ya sanaa za maonyesho. Wasanii wamekuwa wakifanya mazoezi yao kwenye kumbi za bar, watoto wadogo wanaoanza kuingia katika fani wanaanzia kujifunza fani yao katika bar, matokeo yake ni kuanza kutengeneza wasanii wanoingia katika ulevi mapema mno, hii si haki. Zamani sherehe mbalimbali nchini zilisheni shughuli mbalimbali za sanaa za makabila mbalimbali ya nchi hii, kuanzia sherehe ndogondogo kama vile mahafali ya shule mpaka sherehe za Kitaifa mfumo ulikuwa ndio huo, ambao pia ulijenga sana uzalendo. Sasa tumekuwa kama Taifa ambalo halina uhalisia, hata sherehe za muhimu kama za UHURU zinaishia kwa paredi na maonyesho ya Jeshi.

Tanzania ina mitaala mbalimbali ya sanaa, inayoongoza ufundishaji wa masomo hayo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita. Kwa shule za msingi kuna mtaala wa Stadi za Kazi ambao unaonyesha sanaa ivyonatakiwa kufundishwa kuanzia darasa la kwanza, vyuo kama Chuo Cha Waalimu cha Butimba vilianzishwa ili kutoa waalimu wa sanaa, vyote hivyo vimetupwa kapuni. Serikali iko wapi katika sanaa? Nini kinaiafanya serikali yetu kudharau sekta hii ambayo katika nchi nyingine inachangia katika kukuza uzalendo, kujenga maadili, kutengeneza ajira na kuchangia asilimia kubwa katika pato la Taifa?
Leave a Reply

Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com
%d bloggers like this: