HATUPIMI BANDO SIE


KUSIKILIZA EFM 93.7 BONYEZA HAPA

EFM
Kitime-191x300

MKINICHAGUA NI KULA BATA TUUU

Kitime-191x300Ndugu zangu baada ya kutangaza nia wiki iliyopita, na kutokana na kuwa nilikiri sina vipaumbele wala vipaunyuma, nimeungwa mkono na watu wengi sana kisirisiri, nimeungwa mkono na wasomi na wasomaji, viongozi wa makundi mbalimbali yakiwemo ya akina mama na akina baba na wale ambao ni vigumu kuelewa kama ni akina baba au akina mama, pia na makundi mengine hata hayaeleweki maana viongozi wao walikuwa wakivuta sigara ambazo ni wazi hazijatengenezwa kiwandani. Lakini kimsingi waliuliza je, nini kikubwa nitakachokifanya? Maana yote wagombea wengine wameshaahidi watayafanya. Kiukweli ndugu wananchi mimi ndio nafaa, kwanza niseme kwa kiingereza, “I love is my country’ yaani naipenda sana nchi yangu, hivyo siku saba tu za kwanza mtaona mabadiliko ambayo hayajawahi kutokea katika Bongoland yetu. Cha kwanza ni kuwa nitafuta Wizara mizigo nyingi tu, hii itapunguza matumizi ya serikali yangu kwa zaidi ya asilimia 70. Nitabinafsisha wizara kadhaa na kuzifanya ziwe kampuni nakutoa tenda kwa wawekezaji. Nitoe mifano, kuna nchi ambazo asilimia kubwa ya nchi ni jangwa lakini hazina matatizo ya maji, hawa watu wanajua namna ya kutumia maji kwa ufanisi, hivyo basi ni wazi tukipata kamapuni toka nchi hizo kuja kuwekeza kwenye maji, matatizo ya maji katika nchi yetu yataisha katika wiki moja.

Mpaka sasa tumeshaona kuwa watoto wetu wameshasahau utamaduni wetu, ukienda kwenye shule zetu za nasari watoto wanafundishwa kucheza Kwaito na Ngololo, vyombo vya habari vimeamua kuachana kabisa na ngoma zetu za asili, au shughuli zozote za utamaduni, ulishaona luninga ikionyesha kabila likifanya tambiko? Hivyo basi hakuna haja ya kuwa na chombo cha serikali cha kushughulikia Utamaduni ni kuachia makampuni na watu binafsi waendelee tu mambo yameshaharibika, watu waendelee na ishu zao za kanga moko, watajuana wenyewe. Ndugu wananchi, nitaanzisha Wizara ya Displin, Viboko na Nidhamu, wizara hii itakuwa na mamlaka ya kufanya kazi zozote. Nitaanza kwa kutoa likizo ya mafunzo kwa vyombo vya dola. Hivyo vyombo hivyo vitarudi kwenye vyuo vya mafunzo kwa miezi mitatu, wakati jeshi likiwa chini ya wizata hii mpya, litachukua kazi ya kuingia mitaani kuweka displin, baada ya miezi mitatu kutakuwa hakuna daladala kutanua, wala mabasi kwenda mwendo kasi, wala mtu kuchelewa kazini, wala rushwa, wala ufisadi. Hayo ni maamuzi magumu lakini ni kwa faida yetu sote wananchi. Unajua displini ni tatizo kubwa hapa, watu wanaambiwa wasiuze vitu kwa dola wao wanaendelea kutangaza tena hadharani, eti ohh napangisha nyumba kwa dola alfu, ohh nauza kiwanja dola alfu kumi, sasa Wizara ya Displin itasafisha ubishi huu wote, ikiwemo ule ubishi wa kung’ang’ania kuchukua kodi ya mwaka wakati nyumba inapangishwa kwa mwezi.

Naomba mpunguze kushangilia kwanza mtashangilia siku nikiwa naapishwa, ila natoa tahadhari kwa wale waliochukua mgao kwenye tenda za ujenzi wa barabara, maabara, shule na kadhalika, rudisheni mgao kwani itawakosti, nikikujua nafilisi mpaka kuku. Niweke tahadhari mimi sitakuwa naunda tume, nakuja mwenyewe laiv mpaka kwako tunahesabu mali ulizonazo unaanza kunieleza ulipata wapi hela za kununulia VX? Ulipata wapi pesa za kununulia mchepuko BMW? Nakucharaza viboko mbele ya mchepuko wako. Bado nafikiria namna ya kushughulika na vile vyuo vinavyofundisha ujenzi halafu majengo ya madarasa yao ni mabovu, hivi kweli wanatufaa hawa, unasomea uinjinia wa mitaro halafu mabomba na mitaro chuoni hapo imeziba.

Mtaona wazi matumizi ya Wizara zilizopumzishwa yatakuwa yamebaki serikalini bila kazi, hivyo wananchi tunaweza kutumia hela hizo kwa kugawana mara moja kwa mwaka na kila mwananchi kula bata. Nani kama mimi?
Leave a Reply

Your email address will not be published.