full screen background image
images

MUZIKI NA MADAWA YA KULEVYA

imagesKatika siku za karibuni kumefumuka heka heka za kutafuta njia ya kundokana na baa la dawa za kulevya. Katika vurugu hizo majina ya wasanii kadhaa yamejitokeza, mengi sana yamesemwa na kuhusu kukamatwa kwa wasanii hawa,lakini hebu tuangalie Je, jambo hili ni geni katika sanaa? Kama kawaida ukurasa huu huongelea sanaa ya muziki, hivyo nitaongelea kuhusu muziki na madawa ya kulevya. Bila wasiwasi nasema jambo hili sigeni katika tasnia hii. Mwaka 1969 nikiwa sekondari ya Aga Khan Iringa, wanafunzi kadhaa tulianzisha bendi yetu ya shule. Ratiba ya shule iliruhusu wanafunzi kufanya shughuli wazipendazo kwa vikundi kila Jumatano mchana na Ijumaa mchana, kukaanzishwa klabu mbalimbali kama vile, Geography Club, Mathematics Club, Agriculture Club, na kadhalika, mimi na wenzangu wachache tukajikusanya na kuanzisha bendi. Shule ikatupangia sehemu ya kukutana kama ilivyokuwa kwa klabu nyingine na hata kutupatia ‘tape recorder’ kwa ajili ya mazoezi. Siku ya kwanza kuanza mazoezi ya bendi hiyo mwenzetu mmoja ambae nakumbuka alikuwa kahamia mwaka ule kutokea Dar es Salaam alitoa kiberiti kilichokuwa na majani ambayo alisema ni bangi na kuwa yeye hawezi kuanza kupiga muziki bila kuvuta bangi. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona bangi, na pia mara ya kwanza kuona mtu anavuta bangi, na pia mara ya kwanza kusikia mwanamuziki lazima avute bangi kabla ya kuanza muziki. Sikumbuki kuona kitu chochote cha ajabu alichokifanya mwenzetu kimuziki baada ya kuvuta bangi, lakini kesho yake alikuja kulalamika kuwa kuna mtu kati ya wanabendi alimwibia ile bangi hivyo usiku hakulala kwa kukosa bangi ya kuvuta. Jambo ambalo tulibaki kushangaa na kujiuliza kwanini akose usinginzi kwa kukosa bangi?.

Katika maisha ya uanamuziki niliyoendelea hakika nilikuja kukutana na wanamuziki wengi wakivuta bangi kwa maelezo kuwa huwasaidia kupata ‘feeling’ au tuite hisia wakati wa kupiga muziki. Pamoja na wanamuziki wengine kuonyesha kuchangamka baada ya kuvuta bangi, lakini wengi pia waligeuka kero na kuharibu kabisa muziki. Rafiki yangu mmoja ambaye baadae tulikuwa tukipiga nae muziki kwenye bendi ya chuo kimoja alipata hasara ya kurukwa na akili kutokana na matumizi ya bangi, hakuweza kupona tena mpaka alipofariki. Mwaka 1975, sherehe za Sabasaba Kitaifa zilifanyika Iringa, bendi kubwa kutoka Dar es Salaam zilitua katika mji huo, mwanamuziki mmoja alijikuta akivua nguo katikati ya dansi jukwaani katika ukumbi wa Community Center Iringa, baada ya kuvuta bangi, bendi hiyo ililazimika kumrudisha Dar es Salaam kama adhabu. Tukio hilo lilimsaidia akaacha ulevi mpaka alipofariki miaka ya karibuni akiwa na sifa kubwa katika jamaii. Bangi ndio kilikuwa kilevi kilichojulikana sana katika wanamuziki wa dansi Tanzania. Katika miaka hiyo ya sitini kuaanza kuweko umaarufu wa muziki kutoka Marekani. Vijana walianza kuiga uvaaji, utembeaji na hata mila za vijana Wamarekani weusi. Kukatokea kundi la vijana wanaitwa , ‘Yea Man’. Vijana hawa wakaiga hata tabia mbaya za matumizi ya madawa ya kulevya ya Wamarikani, ndipo kwa mara ya kwanza kukaanza kusikika matumizi ya dawa za kulevya mpya heroin. Matumizi ya dawa hizi mpya hayakuingia kwenye anga za wanamuziki wa rumba, labda pengine kwa kuwa wanamuziki hawa hawakukutana na wageni kutoka nchi ambazo zilianza kutumia sana ulevi huu, ila zikaanza kusikika kwenye vikundi vilivyokuwa vikipiga muziki wa kutoka magharibi. Vikundi hivi vingi vikiwa vya vijana waliokuwa wakisoma sekondari vilikuwa vikipiga muziki mchana, kutokana na maadili ya wakati huo kuwa wanafunzi hawaruhusiwi kuweko katika kumbi za muziki usiku. Muziki huu wa mchana uliitwa Bugi, ulipigwa vita sana kuwa unaharibu vijana. Wazazi na viongozi wengi hawakupenda kabisa Bugi, utamaduni wa uvaaji wa viatu virefu kwa wanaume, suruali pana wakati mashati yamebanwa, ufugaji wa nywele ndefu, viliwakosesha usingizi wazee. Hatimae Bugi lilipigwa marufuku katika mkoa kama Dar es Salaam na kusababisha vikundi vingi vya muziki uliopigwa machana kufa. Katika nchi ya Kenya muziki wa huo wa Bugi uliendelea na kulizalisha wanamuziki na vikundi vilivyokuja kupata umaarufu hata nje ya Kenya. Nyimbo nzuri zilizopigwa kwa mtindo wa Funk, kama You can do it ya Slim Ally au Fever iliyotungwa na Ishmael Jingo ni ushahidi tosha wa ubora wa muziki ulipofikia wakati huo Lakini bahati mbaya wanamuziki wake wengine walikuja kuingia katika mtego wa madawa ya kulevya na kufa vifo vya kudhalilika katika umasikini.

Mwanamuziki Steele Beautah alikuwa kiongozi wa wa kundi la Air Fiesta Matata. Kundi hili lililokuwa na wanamuziki 10, lilikuwa bingwa wa muziki wa funk kiasi cha kuweza kupiga na mwanamuziki Mmarekani maarufu duniani wakati ule Miles Davis, Miles alilipenda kundi lile na hata kulialika kwenda kupiga nae Marekani. Mwaka 1971 BBC World service ililitaja kundi hili kama bendi bora Afrika. Bahati mbaya Steele na baadhi ya wanabendi wenzie wakaanza matumizi ya dawa za kulevya baada ya kupata tour ya kuzunguka ulimwengu 1974. Bendi ilianza tour hiyo kwa kwenda kupiga Hong Kong, kisha Uswisi na Uingereza. Wakati wakiwa tayari kwa safari ya kurudi Kenya wakiwa na vyombo vipya na vizuri meneja wao aliyeitwa Mogosti akawaambia ana tatizo la viza kwa hiyo watangulie yeye atawafuata Kenya kwa ndege iliyokuwa inayofuata. Hakuonekana tena, naye ndie alikuwa na fedha na vyombo, ilisemekana alihamia Jamaica, Air Fiesta Matata ikavunjika baada ya hapo. Tatizo la madawa ya kulevya lilimuandama Steele kiasi cha kufikia kulala kwenye mitaro wa maji machafu lakini wanae walimuokota na kumsaidia baada ya muda akaokoka. Mpiga gitaa wa bendi hiyo Matata Sammy Kagenda naye pia alidhurika na madawa aina ya heroine kiasi cha kutokukumbuka hata nyimbo alizotunga mwenyewe, na hata alipoonyeshwa picha zake akiwa kwenye maonyesho alikana kuwa hakumbuki kuweko katika shughuli hiyo. Mazingira yaliyoko sasa ni magumu zaidi kwa kuwa utumiaji wa madawa ya kulevya imekuwa biashara kubwa si jambo la watu wachache kutafuta ‘feeling’. Bahati mbaya Wizara ya Utamaduni, wizara ambayo ingekuwa na nafasi kubwa zaidi kuonyesha njia ya wasanii kupita haipo katika ngazi za chini, mkoani, wilayani au vijijini, hivyo wafanyabiashara ndio wanawaongoza wanamuziki, wanachoangalia ni fedha, hivyo wakiona mfumo fulani unaingiza fedha kwao, hata kama mfumo huo utawaharibia maisha na kuchafua maadili ya nchi kamwe hawatahangaika kubadilisha mfumo. Mwaka 2004 nilikutana na mfanyabiashara mmoja aliyemkaribisha mwanamuziki Mtanzania kufanya onyesho London. Alisema alipata kazi maana mwanamuziki huyo alimwambia hawezi kupanda jukwaani bila kuvuta bangi kwanza. Ili asiharibu biashara alilazimika kutafuta vijiwe vya kuuza bangi amridhishe msanii wake.

 

 
Leave a Reply

Facebook Auto Publish Powered By : XYZScripts.com
%d bloggers like this: