HATUPIMI BANDO SIE


KUSIKILIZA EFM 93.7 BONYEZA HAPA

EFM
Kitime-191x300

NDUGU ZANGU NA MARAFIKI NATANGAZA NIA

Ndugu zangu ninaomba niwataarifu kuwa nimeamua kutangaza nia. Wahenga walisema, msema kweli mpenzi wa Mungu, na mimi ndugu zangu nitakuwa mkweli kuhusu azma yangu hii ya kutangaza nia. Kwanza nianze na ukweli kuwa hakuna mtu hata mmoja aliyekuja kuniomba kutangaza nia, ila mimi mwenyewe kwa kiherehere changu siku hizi, hata nikilala naota nimekuwa kiongozi mkuu wa Bongoland. Huwezi kuamini hata ninapotembea hili wazo linanijia kichwani hivyo nimeona nichukue maamuzi magumu nitangaze nia.

Kitime-191x300Najua mtaniuliza uwezo nitapata wapi wa kuongoza, jamani kwani mliwahi kusikia kuna shule ya Urais, haya mambo mtu yoyote anaweza kikubwa ni kuchaguliwa kwanza, jambo ambalo sioni sababu kwanini hamtanichagua. Najua mtataka kujua nini vipaumbele vyangu. Kama nilivyosema awali msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, kwa sasa sina vipaumbele, kikubwa ni kuwa dili likitiki ndo tutajua nini kiendelee. Ila nawaahidi nyinyi marafiki zangu, wapya na wale ambao nilikuwa nao toka utoto, matatizo yenu yote yameisha, kwa hiyo tuwe pamoja hivyo ni muhimu mkaanzisha ‘Team Chekanakitime’ mpige debe kwa hali na mali niwe Rais, maana nawahakikishia sitawasahau mambo yakijipa. Hivi vitatizo vidogovidogo vya tumilioni kumi, ishirini, mtavisahau kabisa.

Mimi ni mtu ninaependa amani, kwa mfano juzi nimeamulia ugomvi mkali wa wahudumu wawili wa bar ya jirani na kwangu pale Sinza, waliokuwa wananigombania, na nikaonyesha umahiri wangu wa uongozi kwa kuweza kutumia ushawishi wangu, wakakubaliana kuacha ugomvi na kufuata siasa ya ujamaa ya kupeana zamu ya kuwa na mimi. Huu ni mwanga kuwa nikipewa nafasi naweza kusuluhisha migogoro mbalimbali inayoikabiri jamii inayonizunguka.

Lazima niendelee kuwa mkweli, yaani huwa nakesha nikiwaza laif itakuwaje nikiukwaa Urais. Kwanza ishu za misosi, yaani naweza kuagiza kitu chochote kinaletwa, dah mapilau, mibiriani, michips, misamaki, misosej, kila siku asubuhi mayai kwa wingi, mijuisi yaani hata nikiona picha ya msosi fulani kwenye gazeti naagiza tu naletewa. Halafu mambo ya mahala pa kulala, sio shida, bonge ya nyumba bure ya kulala miaka mitano. Nikitaka kwenda popote hakuna foleni, niko ndani ya VX lenye fulu kiyoyozi, ila nikiwa nawapita kwenye foleni nitakuwa nafungua kidirisha juu ya gari kuwapungia mikono wapiga kura wangu. Halafu mimi ntakuwa aina ya Rais ambaye mida ya jioni najitosa kwenye baa mbalimbali kusikiliza malalamiko ya wananchi laiv, na kuona wananchi wanaishije, siku nyingine najitoma kujiachia Msondo au Sikinde wakiwa wanapiga Uswahilini, hizi konset za akina Dully Sykes au Linah ntakuwa nahudhiria, yaani mimi ntakuwa Rais wa watu kiukweli. Mara moja moja napanda bodaboda nielewe laiv nini kinaendelea mtaani,unaona. Uzuri wa Rais mimi sijawahi kuwa kigogo hivyo kimsingi nazijua shida za wananchi kiukweli, siyo nasoma kwenye magazeti tu au naona kwenye TV, hivi saa hizi niko kwenye msoto laiv sijui leo itaishaje.

Halafu niwe mkweli nangoja kwa hamu misafari ya kuzunguka dunia kuonana na akina Obama, kina Buhari tena nikiwa huko ndio ntakuwa naingia kwenye show za akina Tupac, Rihana, PSquare dah mbona sipati picha.

Ila kuna jambo moja kwa sasa sina hela na lazima kufanya promo ili wananchi wanichague. Nawaombeni michango au hata mikopo, nitawalipa kwa riba si unajua tena nikiwa Rais hela itakuwa nje nje. Nikishindwa kulipa nakuuzia kamkoa kamoja unafanya na wewe biashara zako huko au vipi?
Leave a Reply

Your email address will not be published.