HATUPIMI BANDO SIE


KUSIKILIZA EFM 93.7 BONYEZA HAPA

EFM
suspense1

NTAMTOA MTU KONGOSHO

Nipeni pole hali yangu sio nzuri kwa kweli, nimelazwa hapa kwenye zahanati  jirani na kwetu, hali yangu ni mbaya sana, sala zenu zinahitajika. Ajali iliyonileta hapa kwa kweli sijui niiweke katika kundi gani. Unajua ngoja niwahadithie ilikuwaje. Niwe mkweli mimi nilikuwa sijafunga, lakini nilikuwa nasubiri kwa hamu sikukuu ya Iddi ifike maana kwangu ilikuwa ni uhakika wa msosi tena wa nguvu, si unajua baada ya kufunga wafungaji huwa wanakuwa na mioyo ya ukarimu na hivyo  ishu ya  kula inakuwa sio ishu kwa kweli, kila mtaa utakuta kuna watu wanakukaribisha ule, hivyo nilikuwa nasubiri kwa hamu Iddi ifike. Nilikuwa mmoja ya waliokuwa wakifuatilia kwa ukaribu mwezi kuandama,  ungeniona ungedhani na mimi ni mfungaji, kumbe hakuna kitu, akili yangu msosi unaofuatia. Nilisherehekea sana mwezi kuandama nikawa napita mtaa kwa mtaa na ngoma watu wanione kuwa nimefurahia kwa dhati siku kuu hii tukufu.  Siku ya Iddi nikatoa kanzu yangu na kuivaa nikawa nadhifu si mchezo, bwana we si ikaanza mialiko asubuhi mapema, mingine kwa mdomo, meseji za simu, whatsap, watoto wadogo wakatumwa, wote wananiita sehemu mbalimbali kwa ajili ya kula. Ili nisisahahu kila mualiko nikauandika kwenye kakitabu kangu, nikajikuta nimealikwa nyumba tisa, na hapo ilikuwa bado sijaanza kuwatembelea ndugu na marafiki ambao walikuwa wamefunga nikajua kwao lazima kuna msosi. Nikawaorodhesha vizuri nikianzia na nyumba za wenye mkwanja kwanza, nikajikuta nina nyumba kama ishirini na mbili hivi naweza kwenda kula vizuri. Nikapita gengeni nikanunua ndizi kumi, pilipili za alfu mbili nikawa tayari kuitendea haki mialiko yote. Nilianza kwa kuishughulikia mialiko iliyopitia whatsapp, nikaanza nyumba mojamoja nikimaliza naenda nyingine, mkononi mwangu nikiwa nimeshika mfuko wa Rambo wenye pilipili na ndizi, ambazo kwa kweli sikuzitumia maana kote nilikopita kulikuwa na pilipili na ndizi za kumwaga. Nilipofika nyumba ya sita, kwa kweli nilikuwa najisikia sasa tumbo limejaa. Tatizo kila nyumba ilikuwa na vimbwanga vyake, kila mpishi alikuwa katumia ujuzi wake wote, kwa hiyo pamoja na kushiba kupitiliza, wazo la kuachia hivyo vingine lilikuwa gumu sana sikuona uwezekano wa kuacha hata nyumba moja, pia niliona kama ningedharau mualiko wowote ingesababisha nisialikwe tena. Nikajikokota mialiko mingine miwili nikawa hoi,  ikalazimu nikodi bodaboda mpaka nyumbani nikapumzike kidogo, nikafika nyumbani nikalalia tumbo kwa dakika kumi, kisha nikaenda chooni kupunguza kidogo, nikaamua niendelee na kufuatilia mialiko. Kifupi ni kuwa niliweza kuhudhuria mialiko mingine minne tu, ndipo ajali ya kuzimia ilipotokea nilipojaribu kusimama kuelekea mwaliko mwingine. Nimeambiwa nilinyamnyuka kutoka kwenye mkeka lakini nikarudi chini kwa kishindo , waliokuwepo walijaribu kunipepea lakini walipoona sipati fahamu wakaniwahisha hapa zahanati. Kiukweli nilipofika nilipimwa kila kitu nikaonekana sina presha wala kisukari, wala malaria, yutiai, wala taifodi. Kosa walilofanya si wakaniwekea drip, naambiwa ilipoisha nusu chupa nilifungulia bomba ililazimika wanivalishe pempaz maana yake pilau za nyumba kama kumi na mbili ziliamua kuanza kutoka bila mpangilio. Hapo ndipo ilipogunduliwa kuwa tatizo ni kuwa nimevimbiwa, sina ugonjwa wowote. Leo ni siku ya pili bado pilau inatoka, lakini tumbo bado najisikia limejaa gesi  kama ilivyokuwa siku ya kwanza, bado napumulia juu juu, manesi hawana habari na mimi, wananiambia ni ajali ya kujitakia. Ndio maana nawaomba  mniombee, niweze kurudi tena uraiani, na kinachoniumiza akili ni wale watoto wa mtaani kwangu hawana adabu watanitania sana siwezi kushangaa kama watanitungia wimbo, nawaonya kabla sijatoka kikitokea kitu kama hicho namkamua mtu kongosho.
Leave a Reply

Your email address will not be published.